Hebrews 11

Maana Ya Imani

1 aBasi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, na udhahiri wa mambo yasiyoonekana. 2 bMaana baba zetu wa kale walipongezwa kwa haya.

3 cKwa imani tunafahamu kwamba ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, vitu vyote vinavyoonekana havikuumbwa kutoka kwa vitu vinavyoonekana.

Mfano Wa Habili, Idrisi Na Nuhu

4 dKwa imani Habili alimtolea Mungu dhabihu bora zaidi kuliko Kaini. Kwa imani alishuhudiwa kuwa mwenye haki, Mungu mwenyewe akazishuhudia sadaka zake. Kwa imani bado ananena ingawa amekufa.

5 eKwa imani Idrisi alitwaliwa kutoka maisha haya, kiasi kwamba hakuonja mauti. Hakuonekana, kwa sababu Mungu alikuwa amemchukua. Kwa kuwa kabla hajatwaliwa alikuwa ameshuhudiwa kuwa ni mtu aliyempendeza Mungu. 6 fLakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza Mungu, kwa maana yeyote anayemjia Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na ya kuwa huwapa thawabu wale wamtafutao kwa bidii.

7 gKwa imani, Nuhu alipoonywa na Mungu kuhusu mambo ambayo hayajaonekana bado, kwa kumcha Mungu alitengeneza safina ili kuokoa jamaa yake. Kwa imani yake aliuhukumu ulimwengu na akawa mrithi wa haki ipatikanayo kwa imani.

Imani Ya Ibrahimu

8 hKwa imani Ibrahimu, alipoitwa aende mahali ambapo Mungu angempa baadaye kuwa urithi, alitii na akaenda, ingawa hakujua anakokwenda. 9 iKwa imani alifanya maskani yake katika nchi ya ahadi kama mgeni katika nchi ya kigeni; aliishi katika mahema, kama Isaka na Yakobo walivyofanya, waliokuwa pia warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. 10 jKwa maana alikuwa akiutazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu.

11 kKwa imani Ibrahimu, ingawa alikuwa mzee wa umri, naye Sara mwenyewe aliyekuwa tasa, alipokea uwezo wa kuwa baba kwa sababu alimhesabu Mungu aliyemwahidi kuwa mwaminifu na kwamba angetimiza ahadi yake. 12 lHivyo kutokana na huyu huyu ambaye alikuwa sawa na mfu, wakazaliwa wazao wengi kama nyota za mbinguni na kama mchanga wa pwani usiohesabika.

13 mWatu hawa wote wakafa katika imani bila kuzipokea zile ahadi, lakini waliziona kwa mbali na kuzishangilia. Nao walikubali kwamba walikuwa wageni na wasiokuwa na maskani hapa duniani. 14 nWatu wasemao mambo kama haya, wanaonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi yao wenyewe. 15 oKwa kweli kama wangekuwa wanafikiri kuhusu nchi waliyoiacha, wangalipata nafasi ya kurudi huko. 16 pLakini badala yake walitamani nchi iliyo bora zaidi, yaani nchi ya mbinguni. Kwa hiyo Mungu haoni aibu kuitwa Mungu wao, kwa kuwa amekwisha kuandaa mji kwa ajili yao.

17 qKwa imani Ibrahimu, alipojaribiwa na Mungu, alimtoa Isaka kuwa dhabihu. Yeye aliyekuwa amezipokea ahadi za Mungu alikuwa tayari kumtoa mwanawe, aliyekuwa mwanawe pekee awe dhabihu. 18 rIngawa Mungu alikuwa amemwambia Ibrahimu, “Uzao wako utahesabiwa kupitia kwa Isaka,” 19 sIbrahimu alihesabu kuwa Mungu angaliweza kumfufua Isaka kutoka kwa wafu. Na kwa kusema kwa mfano, alimpata tena Isaka kutoka kwa wafu.

20 tKwa imani Isaka alimbariki Yakobo na Esau kuhusu maisha yao ya baadaye.

21 uKwa imani Yakobo alipokuwa anakufa, alimbariki kila mmoja wa mtoto wa Yusufu, akamwabudu Mungu akiwa ameegemea juu ya kichwa cha fimbo yake.

22 vKwa imani, Yusufu alipokaribia mwisho wa maisha yake, alinena habari za kutoka kwa wana wa Israeli huko Misri na akatoa maagizo kuhusu mifupa yake.

Imani Ya Musa

23 wKwa imani, wazazi wa Musa walimficha kwa miezi mitatu baada ya kuzaliwa, kwa sababu waliona kuwa si mtoto wa kawaida, wala hawakuiogopa amri ya mfalme.

24 xKwa imani, Musa alipokuwa mtu mzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao. 25 yAkachagua kupata mateso pamoja na watu wa Mungu kuliko kujifurahisha kwa anasa za dhambi kwa kitambo kidogo tu. 26 zAliona kushutumiwa kwa ajili ya Al-Masihi ni utajiri mkubwa zaidi kuliko hazina za Misri, maana alikuwa anatazamia kupata thawabu baadaye. 27 aaKwa imani Musa aliondoka Misri bila kuogopa ghadhabu ya mfalme. Alivumilia kwa sababu alimwona yeye asiyeonekana kwa macho. 28 abKwa imani akaadhimisha Pasaka na kunyunyiza damu, ili yule mwenye kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza asiwaguse wazaliwa wa Israeli.

Imani Ya Mashujaa Wengine Wa Israeli

29 acKwa imani, watu walivuka Bahari ya Shamu
Yaani Bahari ya Mafunjo.
kama vile juu ya nchi kavu; lakini Wamisri walipojaribu kufanya hivyo, walitoswa ndani ya maji.

30 aeKwa imani kuta za Yeriko zilianguka, baada ya watu kuzizunguka kwa siku saba.

31 afKwa imani, Rahabu, yule kahaba, hakuangamizwa pamoja na wale waliomwasi Mungu, kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi.

32 agBasi niseme nini zaidi? Sina wakati wa kusema habari za Gideoni, Baraka, Samsoni, Yeftha, Daudi, Samweli na manabii, 33 ahambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitekeleza haki, na wakapokea ahadi za Mungu; walifunga vinywa vya simba, 34 aiwakazima makali ya miali ya moto, na wakaepuka kuuawa kwa upanga; udhaifu wao uligeuka kuwa nguvu; pia walikuwa hodari vitani na kuyafukuza majeshi ya wageni. 35 ajWanawake walipokea watu wao waliokuwa wamekufa, wakafufuliwa. Lakini wengine waliteswa, nao wakakataa kufunguliwa, ili wapate ufufuo ulio bora zaidi. 36Wengine walidhihakiwa na kupigwa, hata walifungwa minyororo na kutiwa gerezani. 37 akWalipigwa kwa mawe; walipasuliwa vipande viwili kwa msumeno; waliuawa kwa upanga. Walizungukazunguka wakiwa wamevaa ngozi za kondoo na mbuzi, wakiwa maskini, wakiteswa na kutendwa mabaya, 38 alwatu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao. Walizunguka majangwani na milimani, katika mapango na katika mahandaki ardhini.

39 amHawa wote walishuhudiwa vyema kwa sababu ya imani yao, lakini hakuna hata mmoja wao aliyepokea yale yaliyoahidiwa. 40 anKwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea kitu kilicho bora zaidi ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.
Copyright information for SwhKC